Wakati mmoja palikuwa na tajiri mmoja kwenye mji mkubwa. Tajiri huyu alikuwa mtu mwema na mkarimu. Aliwapenda watu sana na kuwasaidia
kwa mambo mbali mbali. Kwake, kulikuwa na mfanyakazi mmoja wa umri wa katikati. Huyu naye alikuwa mwema sana na walipendana sana na tajiri wake.
Siku moja huyu tajiri alimtuma mfanyakazi wake kwenda sokoni kumnunulia matunda na mboga kwa vile alikuwa anatarajia kupata wageni keshoye. Yule mfanyakazi kwa haraka akamchukua farasi na kwenda kasi hadi sokoni. Kule sokoni kabla ya hata kununua chochote alinunua kikombe cha chai na kukinywa na mandazi mawili.
Baadaye alienda moja kwa moja hadi kwa muuza mboga. Lakini kabla ya kuchukua chochote pale, alishituka na kuanza mbio.
Alikuwa kama ameona mzimu. Alimurukia farasi yule aliyekuwa pale nje na kumwendesha kasi hadi kwa tajiri wake. Tajiri alipomwona anahema na hakuwa na chochote, alimwuliza sababu ya kurudi hivyo.
Yule mfanyakazi hakuweza hata kuongea kwa vile alijawa na hofu kabisa. Tajiri alishituka pia ila akazidi kumwuliza.
Yule mfanyakazi kwa woga na hofu zaidi alieleza kuwa kule sokoni alikuwa amekutana na kifo.
Lo! Tajiri wake alishangaa.
Hakuyaelewa maneno ya huyu mwanamume. Alizidi kumwuliza lakini akaona kuwa hawakuelewana kwa hofu ya mfanyakazi huyu. Lakini kwa kusitasita, aliweza kumweleza jinsi kifo alikuwa amevaa na jinsi alimtambua.
Hapo alimwuliza, “Ungependa basi nikusaidie vipi?”
Yule mfanyakazi akamwambia,
“Tafadhali nipe farasi wako, niende kasi hadı mtaa ule ulio karibu na msitu, ili nijifiche huko kwa siku kadha!”
Basi yule tajiri alimhurumia mfanyakazi wake na akampa farası na kumwagıza aondoke mara moja. Kwa haraka aliondoka ili aweze kufika huko kabla giza.
Hapo yule tajiri naye akamchukua farasi mwingine na kuelekea sokoni. Hakukawia kufika huko. Mara tu alipomkaribia muuza mboga, alimwona mtu ambaye alivaa kabisa kama Kifo, jinsi yule mfanyakazi alivyokuwa amemwelezea.
Hapo akamwuliza. “Wewe ndiwe Kifo?”
Akamjibu, “Ndimi”
“Mbona ulimshitua sana mfanyakazi wangu”
Kifo akamjibu. “Wakati nilimwona nilishituka kumwona hapa kwa sababu tayari tuliagana kukutana leo naye kule kwenye mtaa ulio karibu na msitu. Sikujua kwa nini hakuwa ameenda huko!!!”
Yule tajiri alianza kulia, huku akijawa na huzuni kubwa.