HADITHI ZA MWALIMU BOSCO: Boda

Jere alirauka asubuhi huku akijivuta na kujinyoosha. Alienda mwayo mnene ukikiacha kinywa wazi kwa muda mrefu. Bila shaka alikuwa akihitaji kila chembe cha oksijeni kilichokuwa kwenye mazingira yale.

Mikono ikarefushwa kwenda kulia na kushoto huku akipiga kite na kuguna hata kuku wa jirani waliokuwa mle wakajikusanya baada ya kumkodolea macho, wakapuruka. Kweli kujinyoosha huku hakukuwa kwa kawaida.

Alikuwa akiishi peke yake. Mamaye aliyekuwa hana mwana mwingine alikuwa mara kwa mara akimrai, “Mbona mwanangu hujipatii jiko?” Kwa swali hilo alionekana kutokuwa na muda wa kulijibu. Alikisukuma kipikipiki chake hadi nje ya chumba chake na kukipangusapangusa. Alikuwa amekibatiza jina “Nyati”. Huyu Nyati alikuwa amepakwa marangirangi tofautitofauti. Kama ungemwita manjano, au mwekundu, kijani au mweusi, mweupe au zambarau, hakuna lolote ambalo lingemfaa. Hivyo basi, Nyati alisalia kuwa Nyati.

Bila shaka Jere hakuwa na nia ya kujitosa jikoni na kuuwasha mwenge wowote. Haifahamiki vyema kama alikuwa na kisufuria, au hata kijisahani chochote mle. Kilichokuwa kinaonekana mara kwa mara ni kijikombe kimoja cheupe. Hiki kilijitokeza walau kila asubuhi, pale ambapo Jere alikiandamanisha na kijimswaki, huku akipitisha mkono huku na huku ili meno yanadhifike. Hakuwa mtu wa gumzo mtaani. Waliokuwa wanamfahamu alikokuwa anafanyia kazi ya boda, walisema kuwa alikuwa mtu wa kujinyamazia na kujitazamia.

Baada ya matayarisho haya yote, alikuwa tayari kung’oa nanga. Utayari huu uliashiriwa pale ambapo Nyati alinguruma huku akijitosa kwenye ushindani wa miziki na midundo ya kisasa. Akiwa na kishati chake, kilichokuwa hakijashikishwa mafungo mawili ili kukiruhusu kifua kujidhihirisha, Jere, alimkalia Nyatiwe.

Kweli huyu barobaro alikuwa na siha si haba.

Tangu ajipatie Nyati, alikuwa haambiliki hasemezeki.

Mwaka mmoja uliotangulia, inasemekana kuwa baada ya kukimaliza kidato cha nne (ila wengine walisema kuwa ni cha tatu), alikuwa amejitosa kwenye ulingo wa sintofahamu. Je yalikuwa ni madawa aliyokuwa akiyachuuza, au ni ujangili? Liwe liwalo,  biashara yenyewe ilikuwa si ya kutamanika. Akiwa na wenzake, walikuwa wakifanya mzaha na kifo, kama tu mwogeleaji mpumbavu ajitosavyo kwenye bahari lililojaa mamba. Muda si muda, Jere aliona kuwa alikuwa amesalia peke na pweke. Wenzake wote walikuwa wamelikumbatia wimbi la jongomeo. Hapo hakuwa na jingine ila kuukaidi aliokuwa anaujua na kuomba msamaha kwa wasimamiao usalama. Hapo ndipo akajipatia kipenziwe Nyati.

Masiku hayakupita matatu, akawa ni dereva shupavu. Shule aliyoipitia ilikuwa ni uwanja uliokuwa jioni wachezewa soka ila mchana wakufunzi wa magari na pikipiki walijazana. Baada ya mizunguko miwili mitatu, alikuwa ameshafahamu namna ya kukiwezesha kifaa hiki kisonge mbele. Huu ndio ulikuwa utaratibu wa barobaro kwenye kitongoji hicho. Kufikia jioni, alikuwa mwendeshaji pikipiki hodari na akawa yu tayari kuwabeba abiria. Aliowavutia sana walikuwa ni wavulana wa rika lake na vile vile wasichana wadogo. Hawa huenda walikiona kifua chake, au hata kuufurahia  muziki ambao Nyati alikuwa anaucheza.

Uendeshaji wake Jere ulikuwa ni wa atiati. Mara alimsukuma Nyati kulia, mara kushoto. Aliyakwepa magari kwa kasi akiwaacha madereva wakongwe wakitamaushwa na ugwiji huu mpya. Kasi kwake ilikuwa ni mwenzi; kamwe pole haingemwandama. “Kama wataka nimwendeshe Nyati pole pole, heri ningeenda kwa miguu!” Alisikika akisema.

Miezi ilipita si miwili si mitatu. Yeye na barobaro wenzake walibishana huku na huku kila mmoja akiwashindania wateja. Wote walikuwa wameshajikusanya kuwa kundi lililotambulika kwenye kitongoji kile. Ungethubutu kumkwaza mmoja wao, ungekipata cha mtema kuni.

Jioni moja, rafikiye Jere alijaribu kumkwepa ajuza mmoja aliyekuwa na kijigari kikuukuu. Kwenye harakati zile, akajikwaza kiasi cha kuuramba mchanga. Mara haijulikani jinsi marafikize walifahamu kulihusu janga lile. Kama siafu, walimzingira yule masikini ajuza. Huku wakimsukuma kulia na kushoto wakidai ati kutokana na madaha yake hawajali madereva wengine, walimwibia vijipesa alivyokuwa amejibebea. Hata vifaa vyake vyote hakuvipata tena. Walioneka kutamani kumtendea maovu, ila gari la askari mwitu waliokuwa wanapitia pale, waliposimama, hawa wahuni walitokomea.

Jere na wenziwe walikuwa kwa upande mmoja ni waendeshaji boda wa kujitafutia. Hili lilikuwa jema na hakuna ambaye hangewashukuru na kuwapongeza kwalo. Ila kwa upande mwingine walikuwa ni wanyang’anyi. Walikuwa wamejitwika ujangili ambao uliwaogofya watumizi wengine wa barabara. Kwa vile walinda usalama walionekana kuwapendelea na kutoujali ujangili waliokuwa wanauendeleza, raia walisalia kutokuwa na jingine ila kusalimu amri. Huzuni iliyoje!

Ilikuwa Jumatatu na Jere alikuwa kazini kama ilivyokuwa kawaida yake. Mara kukasikika kuwa mmoja wao, amepatikana kwenye ajali. Ilivyokuwa ada, wakajitosa watatu watatu na waliokuwa kama ng’onda wakajisukumilia wanne wanne kwenye maboda yao. Huku mahoni yakifululizwa, wakajiwekelea kasi wakielekea walikotakikana. Hawakuwa wameenda mbali, kukasikika mlio usiokuwa wa kawaida. Kivumbi kikatanda pale na masauti ya miguno na manung’uniko yakatanda. Safari walioyokuwa wameifunganya ikaonekana kufikia ukingoni. Kwa mbali, chini ya lori moja, kulioneka damu iliyokuwa ikitiririka na vijinyama vilivyokuwa vimekwama kwenye magurudumu mawili ya nyuma. Kwa upande mwingine kulionekana hekaheka za kuwakwamua manusura waliokuwa hawajijui hawajitambui. Mle katikati ya magurudumu kulionekana kuwa na marangirangi kutokana na mabati yaliyokuwa mle. Haikufahamika vyema kilichokuwa kimetukia.

Muda si muda wasamaria wema waliyasimamisha magari yao na kusaidiana kuyaokoa maisha. Mmoja aliwatia manusura wawili kwenye kiti chake cha nyuma, na kuanza safari ya kasi, huku ameyawasha mataa ya gari lake. Akiwa na wenzake wawili, waliwafikisha manusura hospitalini. Hawa wawili, walionekana kuwa kwenye hali mahututi. Akiwa tu pale kwenye kiingilio cha hospitali, mmoja wa hao alisikia akipiga kite na mara akasikika kuishusha yake ya mwisho. Vumbi, damu, tope na hata uchafu uliokuwa mle, ukijiunga pamoja na uvundo wa matapishi au hata kinyesi cha wahasiriwa, vyote vingewahiwa tu na wauguzi. Hawa walijitosa ulingoni. Walioneka kuifanya kazi yao kwa ugwiji wa hali ya juu. Muda si muda, aliyekuwa amesalia hai, aliyefahamika kuwa Jere, alibebwa kwa machera, na kupelekwa kwenye wadi la hospitali ile.

Wiki ya kwanza na ya pili ikapita. Mwezi wa kwanza na wa pili ukafuatia. Jere akawa mle kitandani akizungumza na wenzake. Kwenye wadi ile, walikuwa ni manusura wa ajali za boda. Mmoja alieleza vile kutokana na uendeshaji wake wa kasi, alikuwa amepatwa na magonjwa ya mapafu. Kutokana na baridi kali, na kutojifunika kifua na uso ipasavyo, alikuwa sasa hajiwezi tena, Kupumua kwake kulikuwa ni kwa shida. Alikuwa amefahamishwa kuwa hali hiyo yake haingerejea kuwa sawa tena. Ilimbidi aishi kwa madawa na kamwe asiwahi kuendesha au hata kubebwa kwa boda au gari lolote wazi liruhusulo upepo. Maisha yake yalikuwa yamegeuka. Huyu alikuwa hajatimu miaka ishirini na mitano.

Kwa mwingine, kasi, huku akiwa amepata kileo, ilimwangusha kwenye kijidaraja kilichokuwa na kina kirefu. Akiwa kule chini, aliokolewa na wapita njia akiwa hajifahamu. Hadithi alizozipata baadaye ni kuwa, wasichana wawili aliokuwa amewabeba, wote walizama maji. Mmoja aliwaacha yatima wawili aliokuwa amewazaa mapacha akiwa na umri wa miaka kumi na minne. Huyu naye, alikuwa ameupoteza mkono wake. Alikuwa kalazimika kuishi na uwete huu, maishani.

Jere alikuwa na bahati kuwa hai. Hakumbuki vyema ila huenda alikuwa amewabeba abiria watatu. Nyuma yake kulikuwa na kidosho aliyekuwa amempakata vilivyo na kumfanya kukihisi kijoto mwanana. Huyu hata alikuwa anampapasa na kumfanya kupandwa na hisia. Akiwa kwenye hali hii, alikuwa pia na kasi waweze kufika kule ambako rafikiye alikuwa amepatwa na ajali. Walikuwa wanaenda kwa kasi wamfunze adabu yule aliyekuwa amehusika katika kumwumiza mwenziwe. Yeye Jere hajui kulitokeani! Alikuwa hayahisi maguu yake kwa sasa.

Muda mfupi baadaye alifahamishwa kuwa haya maguu hayangekuwa yake tena. Kutokana na jinsi yalivyokuwa yamepasuliwapasulia, madaktari hawakuwa na jingine ila kuyakata. Angeishi juu ya kijigari cha kusukumwa, maisha yake yaliyosalia.

Mamaye alimshikilia huku akionekana kutokuwa na nguvu tena za kuishi. Huyu mwanaye angejipatia vipi jiko? Alikuwa ameshamwonya mara si haba kuhusu kasi, kuhusu vileo, na kuhusu kujiachilia upepo. Mbona hakuwa na ndewe! Mara tu Jere alipojipatia kijipiki[iki, alimwomba aende kwenye shule njema afunzwe uendeshaji mwema wa kifaa hicho, zikiwemo sheria za barabarani. Kutokana na ujuzi wake maishani, alifahamu vyema kuwa kuzijua sheria za barabarani ni kujilinda, na kuwalinda watumizi wengine wa barabara. Mbona walinda usalama, mbona wasimamizi wa utawala hangewajibika kuhakikisha kuwa sheria zimefuatwa.

Mbona hangewajibika katika kuwaokoa waendeshaji hawa barobaro?

Mbona hakungekuwa na utaratibu kwenye biashara hii ambayo kweli ni ya manufaa kwa wananchi?

Maswali chungu nzima yalimjia huyu mama huku machozi yakimzingira kote ubongoni.

Please follow and like us:

About Author

Related posts

Give a Reply